Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Said Johari ametoa ujumbe maalum kwa Wanasheria pamoja na Mawakili wote wa Serikali kuzingatia ubora katika utoaji wa huduma za sheria ikiwa ni pamoja na kufanya mambo kwa wakati bila kuchelewa ili kuleta maendeleo kwa Taifa
Pia amewataka kutohairisha mambo bila sababu za msingi hali itakayopelekea wateja kukosa huduma bora
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Machi 25,2025 katika mafunzo ya pili ya mwaka ya Mawakili wa Serikali,Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari anasema kumekuwepo na changamoto katika Nchi za Afrika katika utoaji wa huduma kwa haraka na wakati
"Kaulimbiu yetu ya weledi na ubora itakuwa nyuma sana kufikia kama sisi hatufanyi kazi kwa haraka na kwa wakati,huu ugonjwa wa kuchelewa chelewa sio mzuri kabisa unarudisha nyuma maendeleo ya Nchi"Anasema Hamza
"Haya mafunzo yanakwenda kuongeza umahiri katika sekta ya sheria lakini pia tunataka kwenda kufanya kazi zetu kwa haraka na ubora bila kuchelewa chelewa"Ameongeza
Aidha ameongeza kuwa Taifa hili linataka kufanya kazi kwa kasi na ubora ili kufikia uchumi wa kati wa viwango vya juu ifikapo 2050
Kwa upande wake Mwandishi Mkuu wa sheria ofisi ya Mwanasheria ambaye pia ni mratibu wa mafunzo hayo Rehema Katuga anasema kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anajukumu kubwa la kushauri Serikali kuhusiana na mambo mbalimbali ya kisheria
Ametaja mambo hayo kuwa ni pamoja na mikataba,manunuzi,uandishi wa sheria,sheria mpya zinazotungwa na mambo yote yanayohusu Serikali kwa ujumla
Pia anaongeza kuwa pamoja na utekelezaji wa majukumu yao kuwepo na changamoto mbalimbali ikiwemo kuvunjika kwa mikataba hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuwapa ujuzi katika kazi zao
Post a Comment